LAANA ZA
UKOO.
Mara
nyingi unapoenda hospitali, daktari huwa anauliza kama kuna mtu katika ukoo
wako, ana historia ya tatizo hilo na jibu lako humsaidia kujua tatizo lako kwa
undani. Vivyo hivyo laana, mikosi na balaa vinaweza kufuata familia yako kama
zilivyo baraka pia.
Ndio maana
watoto wengi wa viongozi serikali huishia kuwa viongozi, na watoto wengi
wa maskini hujikuta wanaishia kuwa katika umaskini zaidi, ni ukweli ulio
dhahiri kuwa kilichotendwa na baba huwa kinashuka hadi kwa watoto wake. Ukisoma
katika Mithali 13: 22 “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya
mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.” Pia, Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami
sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba
chakula.”
Adamu na
Hawa walipotenda dhambi, hukumu kwa mwanamke ilikuwa hivi, Mwanzo 3:15, Mungu
aliweka uadui kati ya uzao wa mwanamke na uzao wa nyoka. Kwanini
unafikiri Mungu aliweka uadui hata kwa watu ambao hawakuhusika? Jibu ni kuwa
yaliyotendwa na wazazi au mababu wa ukoo yana matokeo sana katika maisha
ya mtu ya leo. 2Timotheo 1:3-5 “…5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na
unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako
Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.” Kumbe kuna uwezekano wa tabia ya
mtu kuunganishwa na familia au ukoo wake. Kama imani yaweza kusafiri kiukoo,
vivyo hivyo na tabia ya kutokuamini au uovu mwingine waweza kusafiri kutoka kwa
mtu kizazi kimoja hadi kingine.
Ndio maana
inawezekana, mtu akajikuta anafanya tabia fulani, na ingawa haipendi lakini
anaendelea kuifanya kumbe ni kwasababu ya ukoo wake. 1Petro 1:18-19 Waweza kumkuta
mtu mwongo, mwizi, mzinzi, mchoyo, mbisho kumbe ni kwasababu ya tabia za
kurithi ambazo zinatokana na laana za familia. Kuna uwezekano mtu akajikuta
hana ndoa ya kudumu, kumbe ni kutokana na laana iliyo katika ukoo.
Ni muhimu kumjua adui unayepambana
naye, watu wengi sana wanajikuta wanapambana na adui wasiyemjua huku wakidhani
wako sahihi, na mwisho hujikuta wana bidii yao haizai matunda, kumbe ni matokeo
ya kupambana na adui usiyemjua. Huwezi kushindana na shetani bila kujua mbinu
zake “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.”
Jambo lingine la Muhimu, maamuzi
yoyote unayoyafanya leo yana matokeo katika maisha yako na ya uzao wako. Ndio
maana wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi ya ahadi Yoshua
aliwaambia, “chagueni hivi leo mtakaye mtumikia” uchaguzi unaoufanya leo una
matokeo mazuri au mabaya katika maisha yako.
Biblia inasema kila andiko lenye
pumzi ya Bwana lafaa kwa mafundisho, kwasababu hiyo tunaweza kujifunza kitu
kutoka katika maisha ya baba wa Imani, Ibrahimu. Mwanzo (11:29-30), ibrahimu
alikuwa hazai maana Sara alikuwa tasa, tunaona pia mwanaye Isaka naye akawa na
tatizo hilohilo la kukosa mtoto kwa mkewe Rebeka (mwanzo 25:21); na jambo hilo
halikuishia hapo kwani na Yakobo alipatwa na tatizo hilohilo.
Pia, kwa namna hiyihiyo ukifanya
yaliyo mema mbele za Mungu, baraka zako hufuatana na uzao wako. Tunaona jambo
hilo kuwa, baraka za Ibarahimu ziliweza kufuatana na uzao wake (Mwanzo 30:1-6;
13:15; 17:7-10) ahadi za Ibrahimu hazikuishia kwake tu bali zilipitiliza hadi
kwa uzao wake. Kumbe baraka zaweza kusafiri kutoka kwa mababu hadi wabibi,
vivyohivyo laana zaweza kusafiri kutoka kwa kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Ndio maana hata Yoabu alipomuua Abneri, ambaye alikuwa awali amesamehewa na
Mfalme Daudi, ile laana ilifika hadi kwa uzao wake.
Utajifunza pia kwa habari ya Yesu,
walipotaka kumuua, wayahudi walitamka wazi kuwa “25 Watu wote wakajibu
wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.” Mathayo 27:24-26
wayahudi walijua ukweli huu kuwa laana zaweza pita kutoka uzao mmoja wa uovu
hadi mwingine, kwasababu hiyo inawezekana unaishi katika mateso leo kwa sababu
ya mambo yaliyopita huko nyuma.
Mungu hapendi kuwatesa wanadamu wala
kuwahuzunisha (Maombolezo 3:33). Lazima usimame kinyume na kila laana katika
familia yako na katika maisha yako, jitenge na kila laana za kutoka kwa familia
au ukoo wako. Balaa, laana na mikosi ya familia yako na ivunjike katika jina la
Yesu Kristo.
BY: EV.ONESMO,
AMOS E.
E-mail:
pasteronesmo@gmail.com -0756391498
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni