Jumatatu, 25 Aprili 2016

USILIPIZE KISASI



USILIPIZE KISASI
 
 

"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana" (Warumi 12:19)
Kuna hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo! Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".

                                              HASARA ZA KULIPA KISASI.
01.Utashindwa.
-Ukiamua kulipa kisasi utashindwa wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili!
2 Wakorintho 10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".

Waefeso 6:12
imeandikwa hivi: "Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".
02.Matatizo hayatakwisha.

-"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya hayataondoka nyumbani mwake"
(Mithali 17:13)
-Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako - Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.
-Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue hakika mabaya hayataondoka nchini mwako.
-Warumi 12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".
03.Unamzuia Mungu kukupigania
-Mungu hawezi kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana".
04.Unajichumia dhambi!

Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo mabaya uliyofanyiwa.
"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).
05.Kutosamehe
Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:
-Yesu Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha mapya.Imeandikwa kwamba, " Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya (2Wakorintho 5:17)
-Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe.
Hatua tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo na amani na jirani zako na ndugu zako.
1. Fahamu kuwa si wewe bali Kristo.
"Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20)
"Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3)
-Mtu akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.
 "Vita hivyo si vyako ni vya Bwana" (2 MAMBO YA NYAKATI 20:15).
2. Mpende adui yako Umuombee
"Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ...." (Mathayo 5:43, 44)
-Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na upendo, kusameheana hakupo.
- Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.
-Ni upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi.
" Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi" (Luka 6:27,28)
3. Samehe na Kusahau.
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii hata mara saba, bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21, 22)
"Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana tuongezee imani" (Luka 17:4,5).
-Ukiishaamua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo katika kinywa chako.Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)
4. Hasira ipeleke kwenye maombi
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26, 27)
"Uchungu wote na ghadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE KWENU" (Waefeso 4:31)
"..... HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu" (Yakobo 1:20)
-Unapoona kuwa kuna jambo limekuudhi, usiwe mwepesi kujibu au kufanya kitu. Tulia kimya na tafuta nafasi uanze kuomba.
       i)Tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako.
      ii)Mwambie Baba jinsi unavyojisikia moyoni mwako, bila kumficha kitu.
     iii)Mwombe kitu ambacho unataka akufanyie katika jambo hilo.
5. Furahi siku zote.
Siri ya ushindi katika matatizo yoyote, inatokana na furaha ya Kristo iliyo ndani ya mtu.
(Wafilipi 4:4)
-" Heri ninyi watakpowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu" (Mathayo 4:11, 12)
-"Upole wako ujulikane na watu wote"
Usiwe mwepesi kumwambia mtu maudhi ya nyumbani mwako, au ofisini mwako. Utajikuta umeingia katika kusengenya na hutafaulu kamwe kujifunza kusamehe.

 
(Wafilipi 4:5)

==============================UBARIKIWE!============================

====================================================================
Pastor. AMOS E.ONESMO-0756391498
E-mail:pasteronesmo@gmail.com
www.amosonesmo.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni