Jumapili, 29 Aprili 2018

KUFANIKIWA KIROHO NA KIMWILI



KUFANIKIWA KIROHO NA KIMWILI
Karibu tujifunze neno la MUNGU muda na wakati kama huu. Leo tunaenda kujifunza somo juu ya “Mafanikio ya kiroho na kimwili”, kupitia mbinu mbalimbali ambazo Mimi napenda kuziita ” Sayansi ya Mafanikio”.
Maana Ya Mafanikio
Kama wasafiri hapa duniani, binadamu tumekuwa tukipigana na kujitahidi kwamba tupate MAFANIKIO ili siku pale parapanda litakapolia basi mtu aweze kuondoka na kuacha alama, kwamba alikuwa amefanikiwa au hakufanikiwa.
Mafanikio halisi yanaanzia kipindi ambacho MTU anampokea YESU Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake.

MBINU ZA KUFANIKIWA KIROHO NA KIMWILI
1. Imarisha fahamu ya Imani
Pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu, Imani ni kutokuwa na mashaka akilini mwako. Maisha yakijawa na Imani kwa kila jambo unalofanya huwezi kukwama.
2Petro 1:5-8

2. Jihesabu kama Mungu anavyokuhesabu.
Hapo sasa ni kuweka nia ya Kristo katika MWENDO. Wafilipi 4:13 ” Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.
Umekubali kutembea kandokando ya mto, basi utakutana na bahari unayohitaji. Nia yako lazima iungwe mkono kwa vitendo. Kutokuruhusu nia itafsiriwe kwa vitendo ndiko kunakomtofautisha mtu anayefanikiwa na ambaye hafanikiwi. Wengi wakiruhusu matendo  yao yafunue nia zao za kufànikiwa watakuwa na maendeleo makubwa.

3. Batilisha fikra za kitoto na uamue kukua.
1wakorintho 13:11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nilisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga, tokea hapa nilipokuwa mtu mzima; nimeyabatilisha mambo ya kitoto”.
1Wakorintho 14:20 ” Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu, lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, Bali katika akili zenu mkawe watu wazima”
Utoto unaozungumziwa hapa ni utoto wa akili, soma Waefeso 4:14.

4. Usikatae fursa za kuwa mdogo.
Mathayo 20:26-27 “Lakini haitakuwa hivyo kwenu, bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu na awe mtumishi wenu; Na mtu yeyote anayetaka kuwa wa Kwanza kwenu na awe mtumwa wenu”.
Anza kuwatumikia wengine kwanza, anza kuwapatia MEMA wanayopenda kwanza na utakuwa umewatawala bila wao kujijua. Angalia wafalme walivyojishusha na walivyofanikiwa, mfano Yesu Kristo. 

5. Unalotaka utendewe watendee kwanza wengine.
Mathayo 7:12 ” Basi yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii”.
Mara nyingi watu WEMA wanabeba mizigo mingi kupita kawaida, kubali kufunua hekima zako kupitia uvumilivu ili uwavute waamini unachoelewa. Au yafaa nini mwanadamu unapenda kuheshimiwa halafu wewe huheshimu wenzako?

6.Fanya jambo zuri unalolihofu.
Hofu na mashaka ni silaha kubwa sana ambayo shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kupata majibu ya maombi ya miujiza yao kutoka kwa MUNGU. Shetani anafahamu kwamba imeandikwa;
” Mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisitasita Roho yangu haina furaha naye” (Waebrania 10:38).
Dawa kubwa ya hofu ni Imani (Marko 11:22). Unapohofia baya usilolihitaji ni ushindani kati ya mwili na imani, iite roho; inajua hilo ni baya, mwili unadai ni zuri. Thibitisha kuwa ni baya kwa kuliacha. Aina za hofu ni pamoja na kukosolewa, kuchekwa, umaskini, kufilisika, kuachishwa kazi,kustaafu, kufiwa n.k

7. Imarisha unyoofu wako/uaminifu.
Ukiwa mnyoofu, mwaminifu utasaidiwa na kila MTU,utawekwa juu ya Mali nyingi na watu wengi (utawaongoza VIZURI). Mwanzo 41:37-44
Katika maisha unaweza kuwadanganya wengi sana, lakini huwezi kuwadanganya hawa wawili yaani nafsi yako na Mungu wako. Ukiwa mnyoofu kwa hawa wawili utapata mafanikio makubwa sana.

8. Ona unachotaka kupitia hicho kidogo ulichonacho sasa.
Kama unataka upate amani, furaha, upendo,afya n.k Ione amani, furaha, upendo au afya hiyo NDANI ya moyo wako kwanza. Hivyo ndivyo kupanda mbegu ya mafanikio kulivyo. Kama moyoni mwa mtu hakuna anachotaka, atakipataje?
Tujifunze kwa Mama huyu katika 2Wafalme 4:1-6
Inawezekana ulikuwa hujui siri ya hicho kidogo ulichonacho, amini kupitia hicho na mafanikio yako yatatimia.
Inawezekana unaomba Mungu akufanikishe kiuchumi lakini huna chochote cha kuanzia, hata Musa wana Waisraeli walipomlalamikia alimwomba Mungu, MUNGU akamuuliza una nini mkononi mwako? (Hicho ndicho kianzio).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni